Sunday, August 13, 2017

TENDAGURU SEHEMU YA PILI




RIWAYA: TENDAGURU
NA: HASSAN O MAMBOSASA
MAHALI: TANZANIA NA MAREKANI




<><><>SEHEMU YA PILI<><><>


"Akili kuchekecha tu, hii inaonesha wazi hawa waliuawa ndiyo wakatupwa kwenye maji na si kingine. Haiwezekani wafe hivihivi tu, ninachokihitaji kutoka kwako kuanzia hivi sasa hakikisha kila picha unayoipiga kwenye miili hii zinafikia mezani kwangu"

"Afande" Amri yake iliitikiwa na Askari yule ambaye alikuwa na kamera pia mkononi mwake alisogea na  kuongeza walau picha zingine za upande tofauti kabisa kwenye miili ile.




_______________________TIRIRIKA NAYO

     Huyu hakuwa na umbo  ambalo linadhihidrishwa kuwa ni amekula miongo  kadhaa kwenye kazi yake,ilionesha ni wazi bado yu wa moto kwenye ajira yake kutokana na jinsi alivyokuwa na damu  joto. Akiwa amevaa shati jeupe ambalo liliofunikwa juu na koti jeusi la suti, chini aliva suruali nyeusi na viatu ambavyo vilijua haswa kufunika nyayo zake na kufanya apendeze. Muundo wa mavazi uliendana haswa kwa jinsi alivyo na hata kuweza kumfanya asiweze kuonana ni mwanausalama aliyekuwa yupo kwenye kazi yake. Bila ya kuambiwa wala kumuona akipewa heshima au kutoka heshima usingeweza kudhani kuwa huyu ni mwenye jukumu la kuhakikishsa usalama wa raia unakuwepo.

      Huyu anaitwa Inspekta Mtela kijana shupavu kutoka ndani jeshi  la polisi, ndiyo kwanza amerejea kwenye kazi yake baada ya kutoka kwenye kozi fupi  nkwenye kambi ya mafunzo ambayo ilimfanya aweze kupandishwa cheo kutoka Mkauzi msaidizi wa polisi hadi kuwa Mkaguzi kamili. Siku hii anakumbana na mauaji ya aina yake yenye kuweka walakini kwenye kila kitu. Kuonekana kwa watu ambao wamekufa ufukweni mwa  bahari ya Hindi. Ilidhaniwa wazi wamekufa maji lakini kwa upeo wake mkubwa hilo suala alipingana nalo vikali, ndiyo maana aliagiza sana mchukuaji wa picha aweze kufanya kazi yake kwa umakini huku yeye akijongea kwenye gari lake ambalo aliliegesha pembezoni mwa barabara.

        Aliketi garini kwa akiwa ameuegemea usukani kwa muda wa dakika kadhaa hadi pale lilipofika gari la wagonjwa ndiyo alishuka tena, muda ambao  Asakri tabibu anawasili hapo akiwa yupo pamoja na gari hilo la wagonjwa na wauguzi kadhaa. Yeye alishuka na kumfuata  akiwa hata hajaanza kuvaa  vitendea kazi  vyake, alimuwahi kabla hajaukaribia mwili na kumvuta pembeni kwa haraka  huyo Daktari Askari mwenye cheo cha ukaguzi usaidizi. Kuonekana kwake  na mwenye jukumu la kufanyia utafiti miili, kulifanya apewe heshima yake kwani ni mwenye cheo kikubwa zaidi yake.

"Jambo afande" Alisalimia huku akikakama kiheshima kutokana na kutokuwa na vazi la kazi ambalo lilimpasa atoe saluti.

"Jambo, Maganga vyema sana jukumu hili limekuangukia kwako wewe. Ninahitaji sana ripoti ya uchunguzi wa hii miili ukiimaliza niweze kuipitia hii itakuwa ni kazi yangu ya kwanza  tangu nirudi tena kazini" Inspekta Mtela alisema.

"Hamna tabu Afande kuhusu hilo, nafikiri imeangukia mikono mizuri"

"Vyema unaweza kuendelea na wajibu wako"

"Afande"

       Mkaguzi msaidizi Maganga aliondoka na kuingia kwenye uwanja  wake wa kibarua, alimuacha Inspekta Mtela akimtazama tu wakati akiendelea na wajibu wake uliyomleta hapo. Kichwa hiki imara zaidi kwenye tafiti ndani ya jeshi la polisi, mwili wake uliyokuwa umeweka muhimili juu yake. Ulisimama imara namna hiyo ukiwa umbali mfupi kutoka lilipo eneo la tukio. Kilikaa namna hiyo  kwa kitambo cha wastani na hatimaye kiliamua kugeuka, viungo vyote vilitazama kule ambapo kuna usafiri wake uliyokuwa umeegeshwa  kando ya barabara.

        Inspekta Mtela alianza kupiga hatua zake kakamavu na ndefu kulisogelea gari alilofika nalo eneo la tukio, kitendo cha kulifikia tu alifungua mlango na kungia ndani yake kwa ajili ya kuondoka eneo hilo. Mlio wa kuwashwa gari  ulifuatia na kisha gari ile yenye vioo vya rangi nyeusi iliingia barabarani, hadhira iliyokusanyika hapo pamoja na mandhari ndiyo mashuhuda pekee wa tukio hilo lililokaa midomoni mwa  watu siku hiyo.

****

        Kijana mwingine kabisa aliagizwa kwa usiri mkubwa na  jopo la wakuu wale  wa wizara ya Maliasili, huyu ni kijana mwerevu aliyejaa busara pamoja na akili nyingi mno katika kupanga mambo yake. Baada ya kupokea taarifa kamili na kiini cha tukio pamoja na kupokea habari za vifo vya wenzake waliyookotwa ufukweni mwa bahari ya hindi, aliamua kuingia kazini kwa namna nyingine aliyokuwa akiijua yeye tu. Huyu alihofia haswa kuweza kuharibika kwa mpango wake ikiwa kazi bado haijatimia, kitendo cha kutoka ofisini kwa wakubwa yeye aliongoza moja kwa moja hadi yalipo makazi yake maeneo ya Ilala. Baada ya kufika ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi  kituo cha kwanza ilikuwa ni kujituliza kwenye kochi, aliegemea sehemu ya  juu ya kochi huku macho akiyatazama kwenye dari la nyumba hilo lililo na feni ambalo  halifanyi  kazi  yake. Hodari huyu mwenye utulivu pamoja na ujasiri alianza kupitisha kila taarifa aliyokuwa ameipata katika mwanzo wa kazi hiyo, kuanzia ripoti kamili hadi kutokea kwa vifo vya wenzake.

       Alipoipititsha taarifa hiyo kwenye halmshauri ya kichwa chake hatimaye alisimama wima kisha akaweka mikono kiunoni, alitazama chini kwa sekunde kadhaa na kisha akainua uso wake juu halafu akauma midomo yake  ya chini. Kamati nzima ya kumbukumbu pamoja na kuweka maamuzi kwenye mambo, ilifanya shughuli maridadi huku mwili ukiwa umetulia vilevile. Hakika suala hilo lilimfanya aumize kichwa haswa hadi kuja kulitimiza kwake kutokana na ugumu uliyopo mbele yake, haikuwahi kutoke vijana shupavu kama yeye kutumwa kwenye kazi moja na warudi wakiwa hawana uhai kwa muda mfupi na  hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza. Tafiti  za kina juu ya tukio hilo tayari zilishafika kwake ,ikiwemo ripoti ya kitabibu, hakueleweka zilifika vipi ilihali muda huo ulikuwa umepita  ni masaa mamwili tu tangu Tabibu wa jeshi  la polisi aweze kufika kule sokoni Feri. Tayari taarifa zote zilikuwa zipo ndani ya kichwa chake na alizielewa vilivyo kiasi cha kutobeba kumbukumbu ya aina yeyote ile.

      Akiwa  hata  bado hajakaa chini simu yake ya mkononi iliita kwa  sauti ya wastani na kumfanya asitishe kuipa wajibu serikali kuu, mikono ilizama moja kwa moja kwenye mfuko wa suruali yake na ukaibuka na simu nzuri ya kisasa.  Aliiweka simu hiyo sikioni na kisha akanena, "Missinzo hapa.................Ndiyo mkuu ripoti nzima nimeipata sasa hivi na ninatarajia kuingia kazini.................hapana sitohitaji mwingine wa kunisaidia kwenye kazi hii nadhani waswahili waliyosema kuwa Panya wengi hawachimbi shimo wapo sahihi kabisa, sipo tayari kitokee kama kilichotokea kwa wenzangu.........Ondoa shaka kabisa mkuu nahitaji kuwa peke yangu kwenye hili.......nashukuru Mkuu"

      Simu ilikatwa na kisha akairudisha mfukoni mwake, huyu ni Israel Missinzo Afisa wa idara ya Usalama wa taifa(TISS) ambaye alichomekwa  maalum kwenye wizara ya maliasili na utalii. Kupewa kwake kwa kazi hii kulikuja baada ya mmoja wa wanausalama aliyepo ndani ya wizara hiyo  kumteua kufanya hilo kwa namna ya kisiri kabisa. Wale wote waliyokuwa wameingia kwenye mpango huo ni wanaidara hii nyeti sana serikalini waliyosambazwa ndani ya wizara hiyo. Mtindo wa kuwaweka wanaidara hawa mithili ya wafanyakazi wa kawaida ndani ya sehemu mbalimbali za serikali, ulikuwa na lengo la kutumika kwenye maeneo mahsusi kama hayo ili kuweza  kulinda maslahi ya serikali na taifa zima kwa ujumla.

       Akiwa ni Mfanyakazi wa ofisi ya wizara jijini Dar kitengo cha teknolojia ya habari, aliitwa  na uchoza mkubwa na kupewa dhima hii.  Huyu hakuhitajia kabisa kujiunga na wenzake kwenye  ajira hii kwani aliona uwapo wa wengi kwenye kazi moja huweza kuzorotesha kazi yenyewe. Ndiyo maana akatoa kauli ya kuwa Panya wengi hawachimbi shimo, akimaanisha idadi kubwa ya watu haiwezi kufikia lengo daima bali kuharibu lengo. Hii  ni kwa mujibu wa maelezo yake na wala haikueleweka nini alifikiria hadi kuamua kusema hivyo,  nia ya kufanya hivi ilibaki moyoni mwake  mwenyewe. Hata Mwandishi wa kisa hiki sikuwa najua aliweka nini fikirani mwake huyu mtu, ya moyoni hubaki nayo mwenyewe  Mwanadamu.

         Baada ya kumaliza kuongea na simu tayari wazo jpaya lilimjia kwenye kichwa chake, haikueleweka aliweka nini  kwenye Kamati kuu. Alitoka tu ndani kwake na kisha akafunga mlango kama ulivyo, Alijongea hadi lilipo gari lake dogo aina ya toyota Harrier kisha kaingia ndani yake. Alitia moto na kuliondoa  hapo maeneo ya Ilala akiwa ni mwenye mwendo wa   wastani, aliamua kutumia njia za panya ili aweze kuwahisha muda na pia kuipiga chenga misururu ya magari katikati ya jiji. Pitapita yake ya njia hadi njia hatimaye alikuja kuibukia Maeneo ya Tabata Kinyerezi, aliongeza mwendo na alikuja kutokea maeneo ya jirani na ulipo  Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere baada ya kuimaliza Tabata. 


        Aliingiza gari lake kwenye barabara ya Mwalimu Nyerere  akawa anaelekea upande yalipo makutano ya barabara ya Tazara,  baada ya mwendo wa mita kadhaa tangu aingie kwenye njia hiyo hatimaye alikata kona upande wa kulia kuingia kwenye barabara inayoelekea uwanja wa ndege. Kituo chake ilikuwa ni  kwenye maegesho ya uwanjani hapo, hapo alizima gari na kisha akachukua miwani ya giza ambayo mara nyingi huwa ipo ndani ya gari. Aliziba macho yake kama vile apendavyo na kisha akashuka na kuongoza njia hadi ndani ya jengo la uwanjani hapo, alifikia sehemu ya mapokezi  ambapo alikutana  na wasichana warembo waliyokuwa wapo ndani ya dhima yao.

"Missinzo ni wewe kweli?" Msichana mmoja miongoni mwa watatu alitamka baada ya kumuona akisogea hapo.

"Sasa unafikiria unamuona mwingine kweli, ni mimi yuleyule leo nimeamua kuja kuwazuru kidogo" Alinena.

"Kweli leo mvua itanyesha haki ya Mungu kama na wewe umekuja kututembelea hapa bila ya kuwa na ziara tu maana wizarani kwa kukupeleka mikoani hawajambo"

"Nina zaidi ya hayo Dorra, kwanza ndugu yangu Mputa yupo ndani kweli?"

"Haswa umemkuta nenda ofisini kwake tu"

"Shukrani wasalimie na wenzio hao wenye kununa tu kama wanalinda mlango wa Jahannam, ngoja nimuwahi Mputa nitarejea tena"  Missinzo alisema hivyo kuwaambia wale Mabinti wawili waliyokuwa wapo kimya alipofika hapo, aliaga na kuelekea  upande ambapo kuna ofisi ndani ya jengo hilo la uwanjani hapo.


        Safari yake haikufika mbali  kwenye mlango aliyohitaji sana kuweza kuwa karibu, kizingitini hapo alisimama na kisha katumia vidole vyake imara alibonyeza kitufe kidogo kilichopo mlango hapo. Alisubiri kwa sekunde kadhaa hadi apale aliposikia sauti ya ukaribisho kutoka kwenye spika ndogo ambayo ilikuwepo jirani kabisa na mlango. Hapo alinyonga kitasa ambacho kililalamika haswa kwa uonevu wake, mlango ulitii amri baada ya kupokea malalamishi ya kitasa na kisha akaingia ndani. Aliurudisha  vilevile huku akiachia mkono wake ambao ulikuwa ukifanya uonevu mno kwa kiruhusu vibanio vya mlango, mandhari pana yenye samani za kisasa ndiyo ilimpokea hapo kukiwa na  mtu mmoja mwenye mwili  wa wastani akiwa amekaa kwenye kiti akiendelea na wajibu wake wa kila siku.

"Missinzo" Mtu huyo aliita

"Mputa" Missinzo naye aliita huku  akipeana naye mkono akiwa bashasha kubwa usoni mwake.

"Wewe Sungura usiyetulia sehemu moja ni adimu sana kuweza kufika eneo kama hili, ukifika kuna Jambo"

"Sijawa Sungura hivi sasa kwani huyo ni mwenye mbio nyingi lakini ni hana pumzi, sasa hivi ni Duma kamili nimefanya upgrade"

"(kicheko kiliwatoka wote kwa pamoja huku Mputa akigongesha mkono na mwenzake) Sema Mtu mzima ambaye mwili wako bado unalilia ujana"

"Niseme nini Kijana ambaye mwili wako unalili zaidi uzee, aisee wazee wamenibebesha gunia jingine ndiyo maana nipo hapa maana ni pa kuanzia"

"(Akijiweka vizuri kwenye kiti) Mchakachaka ushaanza haya sema sasa nikusaidie nini maana mimi ndiyo kituo chenu mkihitaji kuwepo hapa"

"Mputa nafikiri hapa uwanjani una aarifa za kufika wageni wengi sana , sasa nahitaji sana kujua ni wanaelekea wapi na wanachukuliwa na nani. Kuanzia siku ya kwanza kufika hapa uwanjani"

"Ok hakuna shida ngoja nikuitie kijana mmoja muaminifu anaweze kukusaida hilo" Mputa alipotoka kauli hiyo alinyanyua mkonga wa siku ya  mezani kisha akabonyeza namba kadhaa na akasubiri, aliongea aliposikia sauti kwa upande wa pili kutoa amri. Kisha aliushusha mkonga chini, baada ya muda mfupi alifika kijana aliyevaa kinadhifu  ofisini humo.

       Huyu aliwasabahi hao wote aliyowakuta humo akiwa na mchanuo mpana  usoni mwake, baada ya kutoa salamu alisimama hivyohivyo hadi pale alipoamriwa aketi na Mputa. Aliweka egesho lake kwenye kiti kinachotazamana na cha Missinzo na kumfanya awekewe tathimini juu ya muonekano wake na Mwanausalama huyo., kijana huyu macho yote aliyepeleka eneo alilopo yule aliyetoa wito ambao umemjaza hapo kitini.

"Maswi nimekuita hapa, huyu hapa aliyepo mbele yako ni mtafiti maalum kutoka Wizara ya maliasili na utalii. Anahitaji sana kufanya utafiti juu ya wageni wanaomiminika uwanjani hapa kila siku, anzia siku ile ya kwanza ambayo walifika wageni wale hadi leo. Hakikisha tape zote anazipitia huyu hadi anapata taarifa kamili na kupeleka kwa wakubwa zake,nchi hii wageni ni wengi wakiwa na lengo la kiutalii lakini hakuna mapato yanayoongezeka sijui ni kwanini. Missinzo jamaa atakusaidia huyu" Mputa alisema.

"Hakuna shida Mputa" Missinzo alisema

"Nifuate" Maswi alisema na kisha akaanza kuondoka humo ndani, Missinzo alifunga mkia hadi kwenye chumba cha kuongozea kamera ndani ya uwanja huo.


         Mikanda yote iliyorekodiwa ililetwa na kisha ikawekwa kwenye tarakilishi nyingine mahsusi kwa kupita matukio muhimu, zile zenye kuonesha mandhari ya hapo uwanjani ziliendele na wajibu wake kama kawaida kuhofia kupoteza lengo la usalama hapo. Ulianza kuwekwa mkanda wa siku ya kwanza ambapo Missinzo alikaza macho yake kwenye kioo akitazama kwa umakini mno, aliamuru upelekwe kwa haraka ili  kuwahisha muda lakini hiyo haikuathiri azma iliyomleta humo. Mkanda wa kwanza uliishia na kisha ukawekwa wa pili wa siku nyingine, huu ulipelekwa namna hiyohiyo hadi ukaisha. Uliwekwa mwingine  wa siku ya tatu yake   ambapo Missinzo alishaanza kuona mambo yaliyokuwa yakifanana haswa kwenye kila siku, mtu mmoja alitokea mikanda yote ambaye alimtilia  na mashaka.

"Simamisha hapo na mkuze huyo" Aliamuru, yule kijana alitii mari na akafanya vilevile.

"Nasa screenshot yake pamoja na ya gari lake hilo halafu play mwingine" Amri nyingine ilitoka na kijana alifanya kama alivyoagizwa, mkanda wa siku nyingine uliwekwa na mtu akiwa ni yuleyule anayemuona anakuja kupokea wageni uwanjani hapo.

"Piga screenshot kila mkanda wa siku ambazo anafika huyu mtu" Aliweka agizo jingine.


ITAENDELEA!!





WAKATI  TUNAANZA KWA PAMOJA RIWAYA HII, PIA TUNAPENDA TUWAJULISHE YA KWAMBA, RIWAYA NYINGINE  YA NORBERT KAILA TOLEO JIPYA INAPATIKANA  NDANI YA PROGRM YETU PENDWA YA SIMU YA ANDROID IITWAYO HADITHIAPP. INAITWA RALOND NA DESMOND KWA BEI NAFUU TU, PIA RIWAYA YA  SHUJAA AMBAYO ILIWAHI KUKATISHA KWENYE  BLOGU YETU  IPO HUKO UTAUPATA MWENDELEZO WAKE KWA BEI NAFUU. KAMA NI MDAU  WA BLOGU MARIDHAWA, HAKIKISHA UNA  PROGRAMU HII UWEZE KUJISOMEA. KUJIPAKUA FUATA LINK HII>>>>> https://play.google.com/store/apps/details?id=com.developict.hadithi

No comments:

Post a Comment