Saturday, August 12, 2017

TENDAGURU SEHEMU YA KWANZA



RIWAYA: TENDAGURU
NA: HASSAN O MAMBOSASA
MAHALI: TANZANIA NA MAREKANI




<><><>SEHEMU YA KWANZA<><><>


               UWANJA WA NDEGE WA MWALIMU  NYERERE

      Wageni waliyokuwa na asili ya barani Ulaya walionekana wakitoka kwenye mlango maalum, huu ni mtokeo wa wale wote wanaowasili ndani ya uwanja huu. Lilikuwa ni kundi la wazungu waliyovalia mavazi marahisi haswa kwenye macho ya kadamnasi, ilionesha wazi hawa  ni watalii waliyokuwa wapo mapumzikoni na matembezini. Huu  ni mtazamo juu yao lakini hakuna aliyekuwa na uhakika na kile  kilichokuwa kikionekana, ujio wao ndani ya nchi hii ulibaki kuwa  ni habari yao iliyokaa mitimani kwa kila mmoja. kila mmoja alifunika kichwa chake kwa kofia kuhofia haswa jua la jiji  jinsi lilivyokuwa kali. Macho yao  yalistiriwa na miwani ya jua, ilionesha wazi hawakuwa wamezoea mmuliko huu   wa mchana.

         Kundi hili la wageni lilipofika eneo malaum ambapo wenyeji husubiri  kupokea wale wastahikiao  kufanya huvyo, ngozi  nyeupe hizi ziliangaza macho yao katika kila pande ya eneo ambalo walikuwepo. Ilionesha wazi  ni wenye kumtafuta mwenyeji  wao. Mmoja wao ambaye ni mrefu kupita wote ndiyo alinyanyua kabisa kidevu chake kuweza kuona mbele miongoni mwa kundi la watu wenye asili tofauti waliyopo uwanjani hapo kupokea  wageni. Huyu baada ya kuangaza kwa muda mrefu hatimaye aliweza kufikia mwisho wa kufanya hivyo, khatamu aliyoishika ya kutafuta yule aliyekuwa akiwafuata uwanjani hapo aliitumia ipasavyo na hatimaye akatimiza wajibu aliyokuwa  akitakiwa kuukamilisha.

        Mchanuo mwanana aliutoa usoni mwake na kufanya hata meno yake meupe yaliyozingirwa na fizi zenye rangi nyekundu, kuweza kushuhudiwa vilivyo na mandhari pana ya jengo la uwanja huo ukiachilia mbali kadamnasi iliyokuwa haitilii maanani mchomozo wa uso wake. Huyu kilichomfanya hata mabadiliko hayo ya kibebea milango minne  ya fahamu kuwa hivyo, ni  bango  lenye ukubwa wa wastani ambalo lina rangi   nyeupe. Hili lilipambwa na maandishi ya kuwakaribisha wale waliyotakiwa kupokewa. Hakika liliwalenga wao wenyewe waliyokuwa wakihitajika kupata uenyeji jira hilo, alianza kujongea huyu huku akimshika mkono mwanamke  mwenye asili moja naye ambaye alikuwa nyuma yake.  Pangua   watu waliyokuwa uwanjani hapo ndani ya siku ambayo ilipokea wageni wengi, hatimaye walifika mbele ya  kijana mwenye ngozi asilia  ya bara hili. Huyu ndiye aliyekuwa amenyanyua bango lile juu, na alipowaona wageni hao alishusha kisha akawapa tabasamu mwanana.

"Welcome in Tanzania" Aliwakariisha ndani ya nchi aliyopo huku akiwa na sura yenye bashasha kiasi cha kutia mioyo ya wageni hawa hamu ya kutaka kuijua kuhusu nchi hii waliyokuwa wakipitia ukaribisho maridhawa  kutoka kwa huyo.

      Walitoa shukrani zao za dhati kwa kuweza kuingia ndani ya nchi hii, huku wale waliyokuwa na jinsi ya kike miongoni waliyokuwa ndani ya kundi hilo wakimpa kumbatio mwanana huyu mpokeaji.  Bashasha pamoja na tijara za kuonana na mwenyeji wao ziliwafanya hawa waongozane  naye hadi  mahala alipokuwa  ameweka kifuatio chake, kwa pamoja walikaribishwa kwenye kipandio chenye kutumia mafuta. Bila ya hiyana watu hawa waliiingia na safari ikaanza huku wakipiga soga  na aliyekuwa akiwafuata, Kijana yule naye alijua  dhima iliyokuwa imempeleka uwanjani  hapo kwa kuzudi  kuwafanya wageni hao wanogewe na safari yao hiyo.

****

        Ndani ya kikao kwenye moja ya ofisi za kiserikali kulikuwa hakueleweki kutokana na jambo moja kubwa ambalo lilikuwa likiisumbua serikali kwa muda mrefu. Mapato ya serikali yalikuwa ni madogo  kila  kukicha, watu hawa nyeti kutoka wizara ya maliasili na utalii walikaa  hapo wakijadili suala  hilo kwa upana. Nchi hii iliyokuwa na vivutio vya utalii kila kona  siku hiyo ilizidi kuporomoka kimapato zaidi kwenye idara hiyo ukilinganisha na miaka  yote. Kwa mujibu wa idara ya uhamiaji nchini ilionesha wazi kuwa wageni kutoka nje ya nchi walizidi idadi lakini hawakueleweka walielekea wapi. Ilikuwa ni kitendawili kilichozidi vyote vilivyowahi kutegwa na wazee wa zamani hadi wa sasa,  haikupatikana jibu mara moja kutokana na hilo.

       Hoteli nyingi za nchini zilishamiri wageni kutoka nchi mbalimbali waliyokuwa wamepewa kibali cha kuingia wakiwa  na lengo la kutalii, kibaya   asilimia themanini ya watalii waliyoingia wakiwa na lengo hilo hawakuonekana kwenye sehemu zenye utalii nchini. Haikujulikana walifikia sehemu gani ilihali madhumuni yao ya kuingia nchini yalionesha hivyo. Ilikuwa  ni jambo lenye kutatiza haswa na wala hakuna aliyekuwa aking'amua walau kiini chake ilikuwa ni nini.

"Jamani nadhani mnatambua hali halisi iliyokuwa hivi sasa, nchi hii kwa asilimia kubwa tunategemea haswa  utalii kwani huu unaingiza pesa nyingi mno. Cha jabu utaliii huu umekauka kabisa ndani ya nchi na wamebaki asilimia chache waliyokuwa wakiingia nchini kwa lengo la kupitia vivutio vyetu. Cha ajabu wengi wao wanaoingia humu wakisema wanatalii bado haijaeleweka wanakwenda wapi. Suala hili Mheshimiwa huko juu amekuwa si muelewa kabisa akiona sisi wa chini ni wenye kutaka kumfelisha, amefikia hatu ya kuhusisha hili suala na  hila  za upande wa upinzani ndani ya nchi hii" Katibu mkuu wa wizara hiyo alisema.

"Sasa basi  nimewaita hapa kwa mara  moja niwaeleze suala hili nyinyi wakuu kwenye wizara hii, mtambue Mheshimiwa waziri mwenye majukumu mazito ya kuongoza wizara hii hatokuwa na mzaha kabisa na yeyote yule ambaye anahusika na kumfelisha. Amesema hakubali kudhalilika kwa kufutwa kazi kwa ujinga wa wachache, huko juu nimekaripiwa na nikaambiwa lisipopatikana suala hili ufumbuzi basi nitaanza kufukuzwa mimi. Pia mimi sikubali suala hili liwe  ni chanzo cha kuharibika maisha yangu. Nimewaita hapa kuwaeleza hili, sitotaka kusikia utetezi wa mtu yeyote hivi sasa ila nawapa wote majuma  matatu kutoka hivi leo muwe mmekuja na  ripoti kamili yenye kueleza chanzo cha haya yote. Kinyume cha hapo nitaanza na nyinyi kabla ya mimi kufutwa kwa uzembe wa wengine. Nyinyi ikiwa kama wakuu mliyopo chini yangu ni wajibu wenu kuwawajibisha wale wa chini yenu, uzembe wowote ukionekana huko basi wawajibisheni na mje na taarifa kamili. Nimemaliza sina la ziada"  Alipomaliza kuongea alichukua kila kilichokuwa chake na alitoka ndani ya chumba cha mkutano, akiwaacha viongozi hao ndani ya wizara wakitazamana kila mmoja kwa suala hilo.


****

 
         DODOMA

        Habari kubwa iliyokuwa ipo mezani ndani  ya ofisi ya Kamishna wa mkoa ilikuwa ni upotevu wa mabinti wengi, hiyo ilitokea wilayani Kondoa ndani ya mji mkuu wa nchini hapo.  Yalianza ni matukio na kupotea kwa mabinti kila mwezi na matukio ambayo yalifanyiwa uchunguzi  na vituo mbalimbali vya polisi  vya wilaya, lakini kila wakati ulivyokuwa ukisogea ndipo yaliibuka mengine haswa. Mabinti waliyokuwa wakipotea ni rika moja tu na hakukuwa na  umri  mwingine uliyokuwa ni wahanga wa tukio hilo, hii ndiyo ilifanya suala hilo livaliwe njuga kuweza kufikia tamati na hali ya kawaida irudie. Tafiti mbalimbali ndani ya mkoa huo  zilifanywa na polisi wapelelezi waliyokuwa wakiujua weledi wa wajibu wao lakini  haikupatikana jibu sahihi la kila kilichokuwa kikitokea.


         Hii ilifanya wananchi wa kawaida wachachamae haswa na waingiwe na ghadhabu nyingi kutokana na sakata hilo, wengi waliona jeshi la polisi mkoani humo limeshindwa fika kuhakikisha usalama wa raia unapatikana kama kawaida. Mchachamo wa raia wa kawaida ulifanya hadi Kamishna mkuu  wa  polisi mkoani hapo John Faustin aamue kuita kikao cha upesi na wakuu wa polisi tofauti wa wilaya ndani ya jiji hilo, mkutano huo ulifanyika kwenye  chumba cha makutano ndani ya makao mkuu ya polisi jijini  humo. Makamanda wa polisi kutoka wilaya saba tofauti mkoani  hapo waliwekwa ndani ya chumba hicho, hawa ni MaOCD wa  wilaya zote za mkoani Dodoma. Wengi wao ndani ya muonano huu wenye  tija walikuwa ni wenye vyeo vya Urakibu,Urakibu mwandamizi pamoja na Kamishna msaidizi mmoja tu miongoni. Dhumuni la mkusanyiko huo ndani ya chumba chenye kuzungukwa na viti kadha lilishatajwa mbele yao na hapo ilihitajika kusikika mawazo yao juu ya hilo.


       Ugurugushaji dhima ndiyo waliona wazi kiongozi wao aliwadhani kwa jinsi alivyokuwa akigwengwenya meno kila dakika moja aliyoweka kituo katika kulielezea suala lilnaloikabili Dodoma. Uhabithi uliyokuwa umesheheni mkoa mzima pasipo kufanyiwa utatuzi ulitosha wazi kuwafanya  watulie kimya na kusikiliza mzigo mzito wa lawama, ambazo walizihadidi kwa kuziba vinywa vyao hadi pale zilipoisha. Wenyewe pia walitambua  hiyo ilikuwa ni aibu kuu iliyokuwa ikielekea kuhafifisha jeshi zima la polisi, ndiyo maana Mshika hatamu wao aliongea  kwa ukali mno. Kwani matukio hayo yalielekea  kuhakiri jeshi zima  la usalama wa raia.

"Jamani mkiwa kama wakuu wa polisi kwenye wilaya zenu suala kama hili limewashinda wapi? Mna nini  la kunieleza  yaani hata ushirikiano likitokea wilaya hii na kuhamia nyingine inashindikana kweli. Hii  itatia aibu jeshi zima makamanda, na mimi sipo tayari nipokee  aibu hii kwenye mkoa wangu wa kikazi. Nasema sipo tayari na  narudia tena sipo tayari labda awe Kamishna mwengine ila si mimi, unajua wanahabari wakilivalia njuga hili suala tutaweka wapi sura zetu kwa maneno yao ya maudhi yaliyojaa siasa" Kamishna John alifoka kwa nguvu.

      Nani aliyekuwa akipenda sehemu yake ya kazi ionekane ina halafa, jibu ni hakuna  mwenye kuhitaji hilo. Yeyote yupo radhi aonekane jura lakini suala hilo lisionekane. Hakika mtu hulinda upande wake, ndiyo maana Kamishna John alihamaki haswa baada ya kuona hilo lilikuwa likikaribia kutokea. Alipoketi chini baada ya kumaliza kuzungumza Kamanda wa Bahi alinyoosha mkono juu kuashiria ni mwenye jambo, halani alitoa heshima kwa mkuu wake baada ya kusimama tangu  apokee ruhusa.

"Mkuu hili suala kwakweli limechukua sura tofauti ndani ya mkoa wetu, lakini nakuahiahidi hatutokubali kuona likitia doa jeshi la polisi ilihali sisi wenye kuweza kuhakikisha halitokei  tupo" Kamanda wa Bahi alisema.

"Ahadi! Ahadi tu jamani, mpaka lini hamuoni kuwa hali inazidi kuwa mbaya kila kukicha. Ahadi bila ya matimizo ni deni kubwa sasa nyinyi mtakaa na deni hilii hadi lini. Sitaki kusikia hili nawapa majuma mawili ndani ya mkoa huu hao mabinti wote warudi. Kuna mwenye la ziada" Kwa hamaniko alikokuwa nalo Kamishna john hakuna aliyenyanyua kitamkwa chake kusema ni mwenye la ziada.


       Maneno ya mmoja wa makamanda  hao aliona ni hangamaji yaliyokuwa yakihanikiza tu kwenye  halmashauri kuu ya ubongo wake, alitoka ndani ya nyumba hicho cha mkutano akiwa ni mwenye mwendo mkazano akiwaacha  maafisa wa chini yake wakimsindikiza kwa macho. Suala la upotevu wa vigori ndani ya jiji hili lilileta mkanganyiko mzito sana kwa mkuu wao, aliwapa muda ambao hawakuwa wakijua walau waanze vipi kuweza kuingia kwenye mchuano hadi wapatikane wahusika. Ni kitendawili kingine walichoachiwa hawa  wenye wadhifa ndani ya jeshi la usalama wa  raia.


****


        Siku iliyofuata wageni waliendelea kumiminika kama ilivyo ada  kuingia nchini, magari yaliyokuwa yakiwapokea napo haikujulikana yaliagizwa vipi hadi kuweza  kufika hapo. Siku hiyohiyo kikosi maalum cha upelelezi  kutoka ndani ya wizara kilitumwa kwenda kujua walau walipokuwa wakielekea, kikosi hiki kilitoka kwa wale viongozi wa wizara ya Maliasili waliyokaa kikao na Katibu mkuu wa wizara hiyo. Ripoti ilitumwa kwa wakuu wao kama ilivyo kawaida yao na ilielezwa ni wapi wageni hao walipokuwa wakifikia, mujibu wa taarifa zao ilikuwa ni kwenye hoteli kubwa iliyopo jirani kabisa na bahari ya Hindi maeneo  ya Msasani.

       Kikosi hicho cha kujihazahaza kilitegemewa kuweza kuleta taarifa ya kile kilichokuwa kikiendelea lakini nacho baada ya kutoa habari ya  awali hakikusikika tena, kilipotea tu katika mazingira ya kutatanisha yaliyokuwa hayaeleweki ni namna gani. Hakika jambo hili lilipofika kwa wakuu waliyokiagiza lilileta hofu kuu na walibaki ni wenye kuchanganyikiwa kupitiliza. Nyoyo zao zilijawa na woga mkuu ikiwa kiongozi wao aliyewashupalia atajua kazi imeenda kombo, ikiwa vijana waliyohitajia na kukabidhiwa  wameenda na maji. Waliona ndiyo mwanzo wa mvurugo kwenye akili ya mkubwa wao waliyokuwa wakimpa kila intidhamu iliyohitajika. Kuweza kupotea mapato ya utalii tu  yule kizito wala hakujali kuwa wale waliyokuwa wakimpa mbeko  ndiyo hao, yeye aliona  kukongowea kwao kama angepatizingatia si ingekuwa ni  kujiaharibia mwenyewe kibarua.  Siku hii nayo ilimalizika kwa namna hiyo kila mmoja akikiona kitanda kichungu na akatamani hata siku inayofuata isifike, yote ni kutokana na hofu ya siku walizopewa jinsi zilivyokuwa zikipungua.


****


       Asubuhi ya siku iliyofuata ilikuwa na mengine mapya kabisa, haya ni afadhali yale yaliyopita. Jirani na  ufukwe wa bahari ya hindi kwenye eneo mashuhuri kwa kuchuuzwa kwa samaki. Kuliweza onekana miili ya watu ikielea kwenye maji ambayo ilitolewa na kufukishwa hadi ufukweni. Tukio hili la asubuhi na mapema liliibua sura nyingine kwenye jiji  hili lililojaa  hekaheka za kila aina, habari kuu kuliko zote ilikuwa ni kuonekana kwa maiti hizo zilizokuwa hazina jeraha lolote lile zaidi ya kutokuwa na pumzi. Eneo zilipowekwa ziliachwa hapohapo hadi pale polisi walipofika , uchunguzi wa eneo ilipowekwa miili hiyo ulianza mara moja huku utafiti mkuu ukitawaliwa na Askari aliyepo ndani ya vazi  la kiraia. Huyu alisimamia kila kitu na kuhoji baadhi ya watu aliyowakuta hapo  juu ya kuonekana kwake, baada ya kutafiti haswa kwa dakika nyingi alisimama na kisha akasogea kando ambapo kulikuwa na Askari mmoja aliyekuwa yupo  ndani  ya vazi  la kazi.

"Hapa kuna zaidi ya namna" Alimwambia.

"Kwanini unasema hivyo Afande?" Aliulizwa.

"Kufa hii miili bila ya kuonekana alama ya kujeruhiwa wala kuonesha dalili za kuzama maji, kuna zaidi ya jambo hapa"

"Mkuu hayo  umeyabaini vipi?"

"Akili kuchekecha tu, hii inaonesha wazi hawa waliuawa ndiyo wakatupwa kwenye maji na si kingine. Haiwezekani wafe hivihivi tu, ninachokihitaji kutoka kwako kuanzia hivi sasa hakikisha kila picha unayoipiga kwenye miili hii zinafikia mezani kwangu"

"Afande" Amri yake iliitikiwa na Askari yule ambaye alikuwa na kamera pia mkononi mwake alisogea na  kuongeza walau picha zingine za upande tofauti kabisa kwenye miili ile.


ITAENDELEA!!




WAKATI  TUNAANZA KWA PAMOJA RIWAYA HII, PIA TUNAPENDA TUWAJULISHE YA KWAMBA, RIWAYA NYINGINE  YA NORBERT KAILA TOLEO JIPYA INAPATIKANA  NDANI YA PROGRM YETU PENDWA YA SIMU YA ANDROID IITWAYO HADITHIAPP. INAITWA RALOND NA DESMOND KWA BEI NAFUU TU, PIA RIWAYA YA  SHUJAA AMBAYO ILIWAHI KUKATISHA KWENYE  BLOGU YETU  IPO HUKO UTAUPATA MWENDELEZO WAKE KWA BEI NAFUU. KAMA NI MDAU  WA BLOGU MARIDHAWA, HAKIKISHA UNA  PROGRAMU HII UWEZE KUJISOMEA. KUJIPAKUA FUATA LINK HII>>>>> https://play.google.com/store/apps/details?id=com.developict.hadithi

No comments:

Post a Comment