Friday, June 23, 2017

HANJAMU YA MSALITI



RIWAYA: HANJAMU YA MSALITI
NA: HASSAN O MAMBOSASA




 SURA YA KWANZA

    Mvumo  wa kutoka mashariki kuelekea magharibi ulirindima, minazi  pamoja na miti mingine mingine iliyopo  ndani ya mandhari hiyo. Ilipepesuka vibaya kwa mkumbo huo, hali hiyo ilidumu ikiwa na karaha kubwa kwa miti ambayo haikuisha kulalama ikitoa mivumo ya aina yake pale matawi au makuti yalipovamiwa. Karaha kwa viumbe hai waliyojichimbia ardhini, ikawa ni   burudani kwa viumbe hai watembeao juu ya mgongo wa ardhi. Mgeuko wa hali ya hewa kutoka ile ya joto  liletwalo na jua hadi kuwa mpulizo,  ndiyo ikawa hivyo kwa upande wao.

  Wakati huu eneo la kiwambaza  cha juu kabisa la kasri la kifahari, alionekana Mtu mzima mwenye kilemba chenye taji kichwani mwake. Kanzu matata ya rangi ya kahawia ikiwa imemkaa mwilini mwake, miguuni akiwa amevaa kiatu kilichoinuka mbele mithili ya pembe la Ng'ombe. Huyu alisimaama akiwa  ameweka mikono kwenye ruva za sehemu hiyo ya juu,  kando yake kukiwa na vijana wawili waliyoshikilia  magobori. Macho yake aliyaelekeza mbele hatua  takaribani mia moja ambapo kuna ufukwe wa bahari ukiwa na bandari iliyoegeshwa Majahazi kadhaa.
   Alijidhihirisha ni namna gani alivyozama ndani ya dimbwi la fikra,  hata pale kiumbe mwingine alipofika hapo na kumwita. Hakuweza kung'amua hilo, kama vile ni mwenye kutosikia. Kumbe wala haikuwa hivyo, isipokuwa kuwa mbali kinafisi ikapelekea hayo.  Aling'amua kuwa anahitajika na yule aliyepo nyuma yake, hadi pale alipoguswa  begani na kiganja ndiyo akageuka  nyuma kutazama.
             "Muhibu lipi likusibulo maana wananitia shaka  kupitiliza" Aliambiwa na Mwanamke mwenye mavazi ya gharama mwenye taji kichwani mwake, hapo akajikuta mwenyewe akiinama chini kwa sekunde kadhaa   baada ya kuulizwa hivyo.
              "Mahbuba, hababi wa fuad wangu. Mwenye kuisuuza roho yangu, unayependezwa na   mtima wangu. Kipi kukikusibucho?", Aliulizwa kwa mara ya pili.
              "Ewe Malkia wangu, mtawala wa moyo wangu. Sina kingine ila isipokuwa ni hili la Saibah. Wajua umri  unakwenda na sasa umri wake kafikisha eshwiriin, wala haoneshi dhumuni la kutaka Shababi. Yaa Habiba ninaihofu fedhefa kuliko kitu kingine chcohtoe juu ya Binti yangu, kukaa bila ya mume mtoto  wa Sultan Zuad", Alieleza
              "Ni haki yako kuwa namna hiyo ya Habib, ila binti mwenyewe nadhani wamwona.  Hasikii wala haeleweki  ni kipi akifiriacho juu ya hilo, hata mimi naapa kwa jina la Allah  sipo tayari kuona ninapatwa na fedheha kisa yeye"
               "Hakika wewe ni mama mwema kwa binti yako,   basi ni wajibu wako kuongea naye juu ya suala hili. Kama ni kitabu basi wanazuoni kadhaa amepitia na amehitimu mapema kuliko wenzake, je  lipi hilo alisubirilo. Laiti kama ingelikuwa  Makuhani si haramu kisharia, basi ningaliwafuata na kuhitaji jua tatizo la  binti yangu"
              "Afuan yaa Muhibu, madhali limefika kwangu nitakaa niongee naye juu ya hili. Na imani katu hawezi kuniangusha mimi mamaye"
              "Haswaaa! Mama bora haangushwi na bintiye"
             "Huu ni mguu niuinuao hivi sasa ni wa kwake, nikatete naye juu ya suala hili"

    Malkia aliposema hivyo, alimwacha Sultan Zuad akiwa yu pekee  yake mahali hapo. Ahueni ilianza kuonekana   usoni mwake, baada ya kuhakikishiwa hilo suala  na mkewe. Alianza kujihisi ni mwenye aibu kuu kwa kukaa na binti muda mrefu ambaye hakuozwa, fedheha alihisi angeweza kuiepuka majira yeyote yale baada ya kupokelewa vyema na mkewe kwa taarifa hiyo.
    Aliendelea kuwepo eneo hilo akibarizi upepo mwanana wa bahari, alikaa hapo kupunguza joto lakini kipunguzo kilipozidi kiwango. Aliamua kugeuka nyuma na kurejea   ndani, majira hayo ni ambayo hali ya hewa ya baharini ilibadilika ghafla na wingu likatanda kila pande. Kuhofia kushuka kwa  mvua  akiwa ambapo huweza kumpata ikiwa  itanyesha ile ya kiupande, ambayo huweza kumpata ingawa sehemu ya juu imeezekwa.
   Kuingia kwake ndani hakukuonekana  mabadiliko yeyote ya hali hiyo ya mawingu mazito, isipokuwa ni upepo  mkali ukiendelea kuvuma.


****

     Jua kuondoka ghafla na ujio wa upepo mkali pamoja na mawingu mazito, ulipelekea hata mawimbi ya bahari nayo yabadilike ukubwa na kuwa ya kutisha. Yalifika umabali mkubwa tofauti napale ambapo hufikia nchi kavu. Hakika watu walielewa wazi chanzo hiko kikubwa cha maji kuliko vyote  duniani, kimetibuka na wale waliyokuwa wana vyombo vidogo vya uvuvi. Hawakuthubutu kuingia huko, kuhofia kukumbwa na dhoruba kali zaidi wakiwa wapo majini.
   Upande wa katikati, eneo la mbali kutoka ilipo fukwe. Vijana wenye rika tofauti walionekana wakishindana nguvu na mawimbi makubwa. Mashua yao  yalipelekwa kutoka upande mmoja kwenda mwingine, huku maji yakiingia ndani na kuzidi kuleta athari kubwa kwao. Iliwabidi wafanye kazi ya ziada kuweza kujinasua ndani ya kibweka hiko. Vyombo vya kuchota maji pamoja na ulindwaji wa mizigo yao, waliufanya majira yote wakiwa wanaelekea ufukweni.
                 "Kakweree! Shikilia kamba hiyo ya Tanga!", Kijana mmojawapo aliyekaa  nyuma akiwa amejishikilia mkono wake kwenye ukingo wa Mashua alipaza sauti.
                 "Kabwariii! Endelea kuchota maji hivyohivyo jamani, huu mzigo wa leo ni mkubwa kupitiliza. Tuhakikishe wafika ufukweni", Alimhimiza mwingine huku yeye akiiinama chini kwa haraka baada ya tanga kuzunguka kwa ghafla na kufanya mashua yao yabadili mwelekeo.
                 "Turudishe tanga mahali pake, hakuna kukata tamaa",  Aliwahimiza na safari hii akiwa wa kwanza kulishika, wenzake nao walifuatia na kulirejesha lilivyokuwa hapo awali.
       Kutoa maji chomboni na kumwaga nje, kulidumu na hakuna aliyeomesha dalili ya kuchoka.  Daima hiyo ni moja ya chngamoto ya kufanya kazi baharini, kukabiliana nayo ni wajibu na si kuikimbia. Ndiyo maana hawa hawakutaka kurudi nyuma kwenye suala hilo, waliendelea kugangamala nayo
   Wakiendelea hivyo, hatimaye waliweza kufika mahala ufukwe wanauona kwa mbali. Hapo ndipo walizidisha juhudi zaidi hadi wakafanikiwa kufika ufukweni salama, Mashua yao waliyafunga kwa kamba ngumu kisha wakaanza mara  moja kazi ya kutoa mzigo pasipo kujali ukubwa  wa  mawimbi yanayojiri. Kwa uwezo wake Jalali, aliyowajalia hali. Walifanikiwa kuumaliza, hapo walikaa chini wakiwa wanaitafakari  bahari ilivyokuwa.
                    "Weye Fuad isingekuwa   upo,  haki vile tungelizama wote.   Hakika wafaa kuwa nahodha wetu", Kijana mmoja alinena akimtazama mwenzake mwenye asili ya ushombe ambaye ndiye aliyekuwa akiwahimiza.
                    "Bora Makame umeliona, Fuad ni nahodha bora hatujawahi pata kama yeye. Yaani kaweza kutukomboa",  Mwingine alisema.
                    "Yaani nyinyi mkanishukuru mimi muda wote tu, mnasahau kabisa kuwa uwepo wa Jalali. Bila ya huyo wala msingeweza kufikia hii hali, kanijalia kipawa nkakitumia kuwagomboa nyinyi", Fuad alisema.
                     "Hebu oneni kule jamani, si Jahazi ya Waziri   Mkuu ile", Makame alisema huku akionesha kidole ulipo ufukwe wa bahari.
       Loh! Walipeleka huko macho yao, walishuhudia Jahazi lililotengenezwa kwa namna ya kipekeee likiyumbishwa kwa mawimbi sehemu yenye kina kirefu. Wote walijikuta akiwasimama kwa haraka haswa ilipoanza kuanguka na baadhi ya watu majini.
                     "Yarabii wameisha wale", Makame aliongeza huku wakiendelea kushangaa, wakiwa  kwenye hali hiyo. Fuad alikimbia kwa kasi akielekea  yalipo maji, wenzake walipagawa kwa tuko hilo alilolifanya haswa muda ambao bahari imechafuka.
                      "Weee! Fuad weye! Ukumbuke mamayo akutegemea na wala huna baba, usijipalie makaa", Mwenzao mmojawapo alipaza sauti.
    Ikawa ni sawa na kumpigia Mbuzi gitaa, Fuad alishafika kwenye maji ya bahari na akaanza kukimbia kwa kasi kwenye kina kifupi cha maji hadi alipofikkia marefu. Aljitupa na kuzama  ghafla ndani ya maji. Wenzake kwa mbali walibaki wakimtazama  tu, aliibuka kwa mara ya kwanza na  kuanza kuyakata maji kisha akazama tena. Hawa waliyojaa nyoyo za woga walibaki wakimwangalia tu, hadi pale alipofika eneo ambalo Jahazi lipo.
   Bila ya kusita kijana  huyu hodari, aliingia ndani ingawa chombo kimeshaenda mrama. Vijana wenzake wakisubiri hapo walisikia mlio wa pembe ukivuma ambao uliashiria ni hatari. Ulipulizwa mara kadhaa, muda huohuo   hawa vijana  walishuhudia Jahazi likielemea upande mmoja na kisha likaanguka majini. Wote kwa pamoja walisimama kwa ghafla kisha wakaweka mikono vichwani mwao, hawakutarajia kabisa suala la namna hiyo lingeweza kutokea.
                         "Yarabii Fuad hakutoka mule na aliiingia ndani kwenye vyumba vya jahazi lile", Makame alisema kwa sononeko.
    Muda huohuo kikosi cha Asakri kutoka kasrini kiliwasili hapo, hawa walisimama jirani na maji wakiwa hawana lolote lile la kufanya kwa hali iliyopo hapo. Wakiwa namna hiyo, waliona watu wakiibuka kutoka ndani ya maji, hapo ndipo vijana wale waliiingiwa na ahueni baada ya kumuona mwenzao kwa mbali akiwa amemshikilia mtu mwenye asili ya kiarabu. Walishukuru Mungu kwa hilo, wakiona mwenzao hakuwa amekwenda na maji.
      Walimshuhudia Fuad akiendelea kukata maji huku akimsogeza Mzee yule hadi walipofikia eneo lenye maji mafupi. Askari wale waliyowasili hapo nao waliingia majini na kuwasaidia, Kijana hodari akafanikiwa kumtoa Mzee yule kwenye maji akiwa ni yeye pekee aliyesalia. Tukio hilo lilifanya watu waliyokuwa wapo mbali wasogee jirani kumuona huyo aliyekumbwa na dhahama ya baharini.
      Wakiendelea kutazama hayo, Fuad alirejea  kwa  mara nyingine eneo lile ambalo chombo  kilizama. Wenzake ndiyo wakiangiwa na mshtuko wa ajabu, jinsi chanzo hiko cha maji kilivyotibuka ingekuwa ni vigumu kwa mtu kurejea tena namna ile. Hawakuwa na la kuongea walibaki vilevile, alielekea hadi kati ya maji ambapo alipofika aliingia ndani ya kina hicho.
       Muda huo wale walinzi walimpeleka yule Mzee kwenye gari la kuvutwa na farasi. Walianza kumpa huduma ya kwanza huku wachache wakingojea kuingia majini tena kwa Kijana shupavu aliyeamua kuyaweka maisha yake rehani kisa kuokoa wengine. Wakiendelea na zoezi la kumuweka sawa kisiha, kijana alirejea akiwa anawasukuma watu wawili waliyolazwa juu ya ubao. Hatimaye aliweza kuwaokoa wote waliyomo mule ndani, huku wengi wao wakiwa hawana fahamu kutokana na kuzama majini.
    Watoaji huduma waliweza kuthibitisha hakukuwa  na yule ambaye hana uhai miongoni mwa hao wote, wote walisalimika na walihitajika kutibiwa tu wapate siha njema zaidi. Fuad alipomaliza jukumu lake la kujitolea, aliondoka hapo na kuwafuata wenzake waliyokuwa na shaka naye kwa kile alichokifanya.
    Hawakuwa mbali kutoka pale alipokuwa akifanya kazi yake ya  kutotarajia malipo, kutokana na wao kuhama pale walipokuwa awali. Aliwafikia huku akiweka vizuri nguo yake iliyolowana kupitiliza, alikaa chini huku akiwaacha wao wakiwa wamesimama.
             "Wallahi! Fuad wewe ni mtu wa ajabu mno, yaani wenda shindana nguvu na maji yaliyotibuka" Makame alisema huku akimtazama pale chni alipokaa.
              "Sa waona  ngefanya lipi la umuhimu Makame, wangifa wale" Fuad alisema.
              "Yaani ngekuwa mie ningekaa kando, Askari wote hawa wakafanya nini wakati kazi yao nkulinda", Mwingine naye alisema.
                "Weye Thuweni naona nawe ukazidi uoga, yaani mkaogopa nini wakati kila siku twavua tena mara nyingine yakatibuka maji"
                 "Wasema tu ila si kwa yale, yaani ngikaa kando kabisaaa", Thuweni alisema.
                 "Wala uoga hausaidii kamwe, kwanza twondokeni hapa  tupeleke mzigo sokoni. Nkataka kupumzika mimi", Fuad aliposema maneno hayo, alisimama kwa haraka kisha akaanza kujongea kuelekea ulipo mzigo wao.
     Huo ukawa ni mwisho wa kusalia hapo, kuangalia jinsi Majeruhi wale wakipewa huduma ya kwanza na majeshi ya himaya yao. Kuchoka kwa mwenzao aliyefanya kazi kubwa kupitiliza, ikawa  ndiyo mwisho wa kuweka  kituo hapo na muda wa kumaliza kazi  ukawa umewadia.

****

      _KASRINI_
      Mlio wa kinubi ulisikika ukirindima kwenye chumba kilichojitenga, ni ndani ya sehemu ya juu ya Kasri kuu la Sultan Zuad. Ilitokea kwenye chumba chenye  mlango imara wenye mapambo ya dhabau huku ndani kukiwa na pazia lenye nakshi za  vipande mbalimbali vya miti. Ndani ya chumba hicho, alionekana  binti mwenye nywele ndefu kupitiliza. Akiwa amevaa vazi liliuficha mwili wake kwa asilimia kubwa. Huyu ndiyo  vidole vyake  vilikaa kwenye nyuzi za kifaa cha muziki kilichotoa suati maridhawa humo ndani kiasi cha kuburudisha.
     Mita kadhaa kutoka hapo alipo, kitanda kikubwa  chenye nakshi cha dhahabau   kilikaa mkabala naye. Huko ndiyo macho yake yote yalielekea, akimtazama binti mnyange mwenye kuvaa  vazi  refu lililoishia shingoni. Akiwa amevaa mikufu kadhaa ya dhahabu, mwenye nywele ndefu zaidi  zikiwa zipo kwenye kibanio maaluma cha madini ya almasi.  Pembezoni mwake kulionekana mabinti ambao hawakuwa na stara kamili, hawa walishika  vifaa maalum huku wakimpepea kwa taratibu.
   Ulalaji wa kihasara wa mrembo huyo huku akitikisa kichwa kuendana na sauti iliyokuwa ikitoka kinubini. Ulizidi kumpa hamasa mwanamke aliyekuwa akifanyakazi ya kutoa burudani kuendelea zaidi na zaidi, hadi kufikia tani yake. Burudani haikuwa  tu kwa huyo aliyemtolea  macho, bali hadi kwa vijakazi waliyokuwa wakifanya  kazi ya kumpatia upepo mwanana.
     Hali ikiendelea hivyo, sauti ya kutikiswa kwa pazia lile lenye nakshi za miti ilisikika.  Pamoja na hayo hakuna aliyeng'amua hilo kutokana na wote kuweka masikio yao kinubini. Walikuja kung'amua hilo ni baada ya kijakazi mmoja kuweka hadidi kwa haraka. Akiinamisha kichwa chake, hapo  mtoaji ala alikoma mwenyewe na kutazama nyuma yake. Alikutana na uso wa mwanamke mwenye asili ya bara arabu kama ilivyo yule mtolewaji burudani, huyu akiwa amevaa taji la dhahabu kichwani mwake lililounganishwa vizuri na nywele zake ndefu.
                  "Mtukufu Malkia, heshima kwako" Mtoaji burudani naye aliweka heshima kwa Malkia.
                  "Nataka ongea na Binti yangu hima, wote nje", Malkia alinena na wote wakatii wakimwacha binti mwenye  mavazi ghali pekee.
                  "Mama kunani mbona hima namna hiyo?", Binti aliuliza.
                  "Saibah banati wangu, ukiona hivi jua mna zito"
                  "Ukanitia wahka, haya nieleze  mushkeli ii wapi hadi uje namna hii mama"
                  "Mama wajua ukatimiza eshryiin hadi sasa ila hakuna dalili ya mume, ukangoja nini weye. Jua babayo kachoka na hilo, ndiyo maana nipo hapa"
                    "Ummiii! Sijaona wa kuniposa miye, laiti nikaliona huyo wala nisingalikaa hadi sasa ilihali nimemaliza  wanazuoni wote kwa kisomo"
                    "Bint Zuad ukafikiri wanaume  waja wenyewe, inabidi watafutwe nafasi ya kuweza kuongea na wewe walau waweze kutoa posa. Mama ukalishindwa hilo, basi jiandae kuozwa kinguvu na babayo kwani amekupa  wasaa wauchezea"
                     "Umiiiii!"
                     "Nkakwambia hivyo, sasa hivi uongeze na khamsa kwenye umrio ndiyo utajipalia makaa kabisa"
       Maneno hayo yalimfanya Saibah ainamishe kichwa chini kwa sekunde kadhaa akiendelea kuyatafakari, mama yake naye aliuacha ukimya huo akijua ataamka na wazo zuri zaidi kwa ajili yake. Alipitisha ukimya muda wote hadi pale  binti alipoinua kichwa halafu akashusha pumzi, kitendo hicho kilifanya  Malkia akae tayari kwa kusikia uamuzi aliyoufikia.
                   "Umiiiiii!", Saibah alisema huku akikishika kiganja cha mama yake kisha akaendelea, "Nkawa tayari, ila naomba unifanyie jambo. Nataka vijana wote wa mji huu, nchague mwenye"
                    "Sasa hapo ukasema vizuri,  subiri  nifikishe taarifa kwa babayo"
                    "Shukran"
                    "Afuan"
     Malkia aliposema hivyo, aliinuka kitandani alipoketi na  binti yake, alitoka humo ndani akimwacha ni mwenye mawazo. Haikujulikana mara moja kipi kilichomfanya hadi akawa namna hiyo, kama ni hiyo taarifa au ni jambo jingine lolote. Ukweli wa mawazo ya mtu ayajuaye mwenyewe, hakuna mwenye kuweza kutambua kile kilichopo moyoni mwa mtu.

****

    Uchuuzwaji wa mzigo wao, ulifanikiwa vilivyo na wote kwa pamoja. Fuad na wenzake  walimaliza mzigo wao, hawakuwa na kingine chochote kile cha kuwaweka sokoni. Kwa pamoja walirejea yalipo makazi yao, walijongea kwa furaha wakiuacha mji huo kuelekea eneo lenye mashamba mengi ya minazi. Huko walitembea wakivuka mashamba kadhaa hadi wakafika eneo ambalo kila mmoja hushika njia yake, kwakuwa wote kwa pamoja walishagawana mapato yao. Kila mmoja alishika upande wake, wakiahidiana hapo baadaye wangekuja kukutana kwa mara nyingine  tena.
     Fuad alifika  hadi kwenye nyumba ya matope iliyoezekwa kwa makuti, hapo nje alikutana na Mwanamke mtu mzima akiwa sambamba na binti aliyevunja ungo wakifanya kazi mbalimbali za nyumbani. Akiwa na kitoweo kidogo kutoka Baharini, alipokewa kwa furaha na  Yule msichana ambaye alipeleka ndani hima. Aliamua kuketi kwenye mkeka majira ambayo binti kaingia ndani, alishusha pumzi ndefu kutokana na uchovu aliyokuwa nao
                   "Baba pole sana, nkajua kazi ya huko ni nzito sana", Mama aliyepo hapo alisema.
                   "Si hivyo mama, yaani leo nkafanya kazi nzito kupitiliza zaidi hata ya hii ya kila siku", Fuad alisema.
                   "Ipi  hiyo?"
                   "Sayidina  Sulaiman leo akazama  majini yeye na watu wake, nkawaokoa wote  mama tena bahari ilivyochafuka imenchosha mno"
                    "Mwanangu  ni hatari hiyo, maji ya namna hiyo si ya mchezo. Nkakukanya sasa hivi, usirudie tena hilo baba. Nkakutegemea"
                    "Wao pia wataka kuishi, ndiyo maana nkatoa msaada. Wangifa nngehisi nna hatia mama"
                    "Ukawa kama babayo we mwana, akafa kwa ajili ya  mwingine na wala hajaliwi mwanangu"
                     "Sitajali juu ajali au hajali, ilimradi nkafanya ihsani. Itaja nisaidia  maishani. Umiii! Hakuna aijuaye shida, saidia usaidiwe"
                     "Haya mwanangu, ila ukumbuke   twakutegemea. Babayo aondoka kisa kusaidia watu, wala sijaona akilipwa fadhila sisi familia yake. Sultan Zuad akafahamu vizuri, waarabu wale nkawachukia mno"
                     "Yaliyopita si ndwele Umiii, tugange yajaye. Nshasamehe hilo, wala sina neno nao"
        Yule binti aliyetumwa ndani alirejea mara moja, akiwa ameshaweka mzigo ule. Alijiunga nao mkekani hapo, kuendelea kupiga soga Waliteta huku wakicheka kwa furaha kuu, kuonesha ni namna gani walivyo na   maisha ya raha ingawa hayakuwa yenye ufahari mkubwa.  Furaha ya familia iliyokuwepo ingawa wapo kihali duni, hiyo haikuwa sababu ya wao wasiendelee kufurahia  kila siku yao ya maisha.  Wakiendelea kupiga domo, kulisikika tarumbeta kubwa ambalo mara nyingi hutoka kwenye sehemu ya nje ya ukuta  wa kuingia kasrini. Lilipulizwa mara kadhaa na kuwafanya wote wakae kimya,  baada ya hilo  kulipita ukimya kisha likasikika tena likilia kwa nguvu.
                      "Kuna jipya likatangazwa huko", Fuad alisema.
                      "Huenda, tusubiri wakaja huku wale baadaye", Mama yake  alisema.



TUWIE RADHI KWA KUWA KIMYA KWA MUDA MREFU, KARIBU TUTAREJEA ILA UKIMYA WETU USIWE  CHANZO CHA WEWE KUKOSA BURUDANI YA KIPEKEE KUTOKA MARIDHAWA. TUNAKULETEA  HANJAMU YA MSALITI, KITABU CHAKE NAKALA  LAINI KIPO HIVI SASA KWA SHILINGI 3000 TU. WASILIANA NASI KUPITIA WHATSAPP 0713 776843 UJIPATIE  NAKALA LAINI YAKO MWENYEWE

No comments:

Post a Comment