RIWAYA: HANJAMU YA MSALITI
NA: HASSAN O MAMBOSASA
SURA YA KWANZA
Mvumo wa kutoka mashariki kuelekea magharibi ulirindima, minazi pamoja na miti mingine mingine iliyopo ndani ya mandhari hiyo. Ilipepesuka vibaya kwa mkumbo huo, hali hiyo ilidumu ikiwa na karaha kubwa kwa miti ambayo haikuisha kulalama ikitoa mivumo ya aina yake pale matawi au makuti yalipovamiwa. Karaha kwa viumbe hai waliyojichimbia ardhini, ikawa ni burudani kwa viumbe hai watembeao juu ya mgongo wa ardhi. Mgeuko wa hali ya hewa kutoka ile ya joto liletwalo na jua hadi kuwa mpulizo, ndiyo ikawa hivyo kwa upande wao.