RIWAYA: DHAHAMA
MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA
SIMU:+255713776843
+255762219759
WHATSAPP:+255713776843
SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINE
SEHEMU YA KWANZA!!
SURA YA KWANZA
Hali ya simanzi ilikuwa imetawala katika eneo zima la kasri la kupendeza la kifalme katika himaya ya Majichungu inayopatikana katika bahari ya hindi, himaya hii ya kijini iliingia katika huzuni baada ya mfalme wao kuwa katika harakati za mwisho za maisha yake. Mfalm huyu aitwaye Zulain mwenye miaka yapata elfu tatu alikuwa katika ugonjwa kwa muda wa miaka kumi sasa leo ndiyo dalili za kufikia mwisho wa uhai wake zilionekana dhahiri kwa majini wote wa hapo kwenye kasri hilo. Akiwa kalala kwenye kitanda chake cha thamani kwa muda wa miaka kumi kutokana na ugonjwa uliokuwa unamsumbua ambao haujulikani, kwa mara ya kwanza aliinuka kitandani ghafla akakaa kitako kisha akasimama akaelekea kwenye kiti chake cha enzi akiwaacha watumishi wake wakiwa na simanzi sana. Kuugua mfalme kwa muda mrefu kisha kuinuka ghafla ni dalili tosha ya kuwa siku za mwisho za miaka yake zimekaribia, hivyo hata watumishi wa ndani ya kasri hili walitambua kuwa siku za mwisho za uhai wa mfalme wao zimekaribia.